17 Mei 2025 - 23:22
Source: Parstoday
Umoja wa Mataifa: Uhaba wa chakula Gaza umefikia kiwango cha janga la njaa

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, uhaba mkubwa wa chakula katika Ukanda wa Gaza umefikia kiwango cha janga la njaa.

Mtandao wa Kimataifa wa Kupambana na Migogoro ya Chakula umetangaza kuwa uhaba mkubwa wa chakula huko Gaza umefikia kiwango kibaya zaidi cha "janga na njaa."

Haya yamo katika ripoti ya kila mwaka ya mtandao huo kuhusu matatizo ya chakula duniani, ambayo ilichapishwa siku ya Ijumaa.

Mtandao wa Kimataifa wa Kupambana na Migogoro ya Chakula ulianzishwa mwaka 2016 na unaleta pamoja Umoja wa Ulaya, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Marekani, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Benki ya Dunia, kwa mujibu wa tovuti ya FAO.

Mtandao huo umesema kuwa, mwaka 2024, watu milioni 295.3 katika nchi 53 kati ya 65 au maeneo yaliyoshughulikiwa na utafiti huo walikabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula. Idadi hii takriban ni watu milioni 13.7 zaidi ikilinganiishwa na mwaka wa kabla yake wa 2023.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula iliongezeka kwa mwaka wa sita mfululizo mnamo 2024, na kwamba sababu kubwa zaidi ya uhaba wa chakula ni "migogoro."

Kwa upande mwingine, mtandao huo ulibainisha kuboreshwa kwa usalama wa chakula katika nchi 15, zikiwemo Afghanistan, Kenya, na Ukraine.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha